Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bangladesh yafichua siri ya kuboresha afya ya mwanamke na mtoto

Bangladesh yafichua siri ya kuboresha afya ya mwanamke na mtoto

Bangladesh iko katika mwelekeo sahihi ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto kutokana na mkakati wake wa kuwekeza katika sekta ya afya ya umma licha ya kuwa na changamoto zingine za uchumi na mazingira. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Balozi Abdul Momen, mwakilishi wa kudumu wa Bangladesh katika Umoja wa Mataifa amewaeleza washiriki wa tukio maalum la kuweka mweleko mmoja wa utetezi wa afya ya mwanamke na mtoto kupitia kauli mbiu Kila mwanamke Kila mtoto mjini New York kuwa, changamoto za kiuchumi, kimazingira hazijazuia nchi hiyo kuwekeza katika afya ya watu wake hususan wanawake na watoto. Imeelezwa kuwa utashi wa kisiasa ndio umewezesha idadi ya vifo vya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano kupungua kutoka zaidi ya Laki Tano mwaka 1990 hadi Laki Moja na Elfu Thelathini na Wanne hii leo.

(SAUTI YA Balozi Momen)

“Tunachohitaji ni utashi sahihi wa kisiasa, jitihada zilizoratibiwa, hatua zenye mwelekeo na nyongeza ya rasilimali kwa siku zaidi ya Mia Tisa zilizobakia na baada ya hapo. Kwa kuongeza uwezo wa watu kupata huduma za msingi za afya, kuwapatia wakunga mafunzo ya msingi na huduma ya kupima damu na chanjo, tunaweza kusaidia hali kuwa bora zaidi.”

Mwenyekiti mwenza wa afya ya mtoto katika ushirikiano wa malengo ya Milenia, Leith Greenslade akizungumza kwenye shughuli hiyo amesema misingi ya Afya ya kampeni ya Kila mwanamke Kila mtoto inaanza kuzaa matunda kwani Bangladesh, China, Ethiopia, Malawi, Misri na Indonesia zimepunguza vifo vya watoto kwa asilimia Sitini kutokana na utashi wa kisiasa.