Baraza la Usalama lakutana kuhusu hali Mashariki ya Kati na suala Palestina

23 Julai 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kujadili hali Mashariki ya Kati likiwemo suala la Palestina. Joshua Mmali ana taarifa zaidi. Mratibu maalum wa harakati za amani Mashariki ya Kati ambaye pia ni mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kwenye ukanda huo, Robert Serry, ameliambia Baraza la Usalama ya kwamba, wakati hali katika ukanda huo inapozidi kuwa tete kwa sababu ya janga la kibinadamu linaloendelea kuvunda zaidi nchini Syria na hali ya kisiasa iliyopo sasa nchini Misri, harakati za amani ya Mashariki ya Kati zina umuhimu mkubwa kwa hatma ya ukanda mzima.(Sauti ya Robert Serry)

 Kuendeleza harakati za amani na misimamo inayochochea amani baina ya pande zote, kutakuwa na matokeo muhimu ya kikanda kisiasa. Lakini kuendelea kuwepo mkwamo kutafanya matumaini ya kuwepo makubaliano ya suluhu la mataifa mawili kudidimia zaidi. Katika juhudi za kuanzisha upya mazungumzo kati ya pande hizo mbili, majira yanatakiwa kupewa umuhimu.

Bwana Serry amesema pande zote zitatakiwa kufanya maamuzi muhimu sana katika siku zijazo, huku viongozi wa Israel na Palestina wakitakiwa kupata uungwaji mkono wa watu wao. Amesifu juhudi ambazo zimekuwepo za kuongeza upatanishi kati ya pande hizo mbili, lakini akaongeza kuwa juhudi zaidi zinatakiwa katika siku zijazo, hata kabla ya mkutano wa marais wa Baraza Kuu mwaka huu.