Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Mali hawapo kwenye daftari za wapiga kura:

Wakimbizi wa Mali hawapo kwenye daftari za wapiga kura:

Wakati uchaguzi wa urais nchini Mali ukiwa umepangwa kufanyika mnamo Jumapili Julai 28, Shirika la Kuhudumia wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, UNHCR, lina hofu kwamba idadi kubwa ya wakimbizi huenda wasipate nafasi ya kufurahia haki yao ya kidemokrasia. George Njogopa na taarifa kamiliKulingana na UNHCR pamoja na kwamba zaidi ya wakimbizi 19,000 walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi ujao wa Mali, lakini hadi sasa ni nusu tu ya majina yaliyoonekana kwenye daftari la wapiga kura.

Shirika hili la kuhudumia wakimbizi  limeelezea wasiwasi wake kutokana na kasi ndogo ya kutoa vitambulisho vya kupigia kura hatua ambayo inaweza kusababisha wakimbizi wengi wasipige kura. Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR .

 (SAUTI YA ADRIAN EDWARD)

“Ni muhimu kwa mamlaka husika zikaanza kutoa majina hayo haraka iwezekanavyo. Jambo hilo ni muhimu likafanyika kwa haraka kwa vile kambi nyingi za wakimbizi ziweka katika maeneo ya mbali ambako inaweza kuwa ngumu kwa sababu ya hali ya mvua inayoweza kuanza kunyesha.

Mamlaka za Mali zimetuarifu kuwa inaangalia uwezekano wa kuwezesha wakimbizi hawa kupiga kura kama itajitokeza tatizo la kuchelewa kwa vitambulisho vyao.

 Wajibu wetu kwenye uchaguzi huu ni kuhakikisha kwamba tunawawezesha wafungwa hao kutimiza haki zao kwa kushiriki kwenye uchaguzi na kutoa fursa sawia ambayo itawezesha uchaguzi huu unafanyika katika mazingira mazuri.”