Mapigano mapya Darfur yawaacha watu 250,000 walolazimika kuhama bila chakula: WFP

23 Julai 2013

Machafuko mapya katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan yamewalazimu zaidi ya watu 250,000 kutoroka makwao na kuacha kila kitu nyuma tangu mwazoni mwa mwaka huu, kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Chakila Duniani, WFP. Alice Kariuki na taarifa kamili(RIPOTI YA ALICE KARIUKI)

Machafuko  hayo ya yaliyodumu kwa miongo kadhaa, yanaripotiwa kuchukua sura mpya katika siku za hivi karibuni kufuatia kuibuka kwa mzozo wa kikabila unaohusishwa na ugomvi wa rasiliamali ikiwemo ardhi na mali asili.

Machafuko hayo mapya yamesabisha idadi kubwa ya wananchi kukosa makazi na wengi wao kukimbilia maeneo ya mbali kwa kuhofia usalama wa maisha yao.

Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la chakula WFP nchini Sudan Adnan Khan amesema kuwa hali ya wasiwasi inaendelea kuongezeka katika eneo hilo na  kuwa kadri mapigano yanavyoendelea kuchacha yanaongeza tishio la kuzuka kwa baa chakula katika siku za usoni.

Hali halisi ya mapigano hayo yanaripotiwa kuendelea kuchukua sura mpya hatua ambayo inaongeza ugumu wa kusaka suluhu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linasema kuwa kiasi cha watu 250,000 wako kwenye hali ya kuhangaika kutokana na kukosa makazi na kati yao, watu 30,000 wamevuka mpaka na kukimbilia nchi jirani ya Chad.