Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili hali ya kisiasa Burundi

Baraza la Usalama lajadili hali ya kisiasa Burundi

TAARIFA YA JOSHUA MMALI

Bwana Onanga-Anyanga, ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Burundi, BNUB, ameliambia Baraza la Usalama kuwa ili kuandaa uchaguzi wa amani, uwazi na haki, mazungumzo yanatakiwa yafanyike kuhusu kuweka mazingira bora kwa ajili ya uchaguzi mwaka 2015. Bwana Anyanga amesema serikali na wawakilishi wa ofisi yake wameanza kufanya maandalizi ya kuanza mikutano kama hiyo ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.

Ameongeza kuwa kurejea kwa wanasiasa maarufu Burundi ni hatua muhimu na ishara inayotia moyo kuhusu wahusika wote wa kisiasa kushirikiana kwa ajili ya uchaguzi wa amani, huru na wa haki.

Bwana Anyanga pia amesema, Umoja wa Mataifa unakaribisha hatua ya rais wa chama tawala, CNDD-FDD na viongozi wa makundi ya vijana kutoa taarifa za kukataa kuunga mkono vitendo vya ghasia.

SAUTI YA ANYANGA

Amesema, kwa ujumla, Burundi inaendelea kufurahia usalama na utulivu, ingawa visa vya mapigano baina ya vikosi vya serikali na makundi yenye silaha vimekuwepo, vikiwemo na makundi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.