Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya haki za binadamu inafuatilia hali Guinea

Ofisi ya haki za binadamu inafuatilia hali Guinea

Ofisi ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa imesema hali ya utulivu inaonekana imerejea inafuatilia nchini Guinea baada ya siku tatu za ghasia za kikabila, kati ya kabila la Guerze na Konianke kwenye kata ya Koule, kwa karibu kilomita 45 kutoka mji wa Nzerekore, ambazo zilianza mnamo Julai 15.

Mapigano hayo yanadaiwa kuzuka kutokana na ugomvi baina ya watu watatu, pale wawili wa kabila la Guerze walipompiga na kumuua kijana wa kabila la Konianke baada ya kumtuhumu kwa kuiba mali kutoka stesheni ya mafuta walipokuwa wakifanya kazi.

Msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Rupert Colville amesema ghasia hizo zilienea hadi maeneo mengine ya jimbo la Forestière, na kusababisha mauaji ya watu wapatao 57, na kuwajeruhi wengine 163, pamoja na kuwalazimu mamia yaw engine kuhama makwao na kutafuta hifadhi katika kambi za wakimbizi Nzerekore na Beyla.

Serikali ilitangaza amri ya watu kutotoka nje mnamo Julai 16 na kutuma ujumbe wa mawaziri kwenye eneo hilo kwa ajili ya kuwezesha mazungumzo ya upatanishi kati ya makabila hayo mawili. Ofisi ya haki za binadamu imepongeza juhudi za serikali na vikosi vya usalama kurejesha utulivu, na kukumbusha kuhusu haja ya kuheshimu haki za binadamu wakati wa operesheni hizo.