Mbinu mpya zahitajika katika utunzi wa sera za uwekezaji: UNCTAD

19 Julai 2013

Kamati ya biashara na maendeleo katika Umoja wa Mataifa, UNCTAD imetoa mwelekeo mpya wa uwekezaji dunani wenye lengo la kuhakikisha hatua zozote za uwekezaji zinachochea ukuaji uchumi jumuishi na maendeleo endelevu. Mwongozo huo upo katika muhtasari wa toleo kuhusu makubaliano mapya ya kimataifa kuhusu uwekezaji uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya semina ya uwekezaji iliyofanyika Finland ambapo kwa sasa umewekwa bayana. Muhtasari huo unajadili mabadiliko ya sasa ya mwelekeo wa uwekezaji hususan kwenye utungaji sera yaliyochochewa na mabadiliko halisi ya kiuchumi na midororo kadhaa ya kiuchumi ambayo imedhihirisha umuhimu wa ukuaji uchumi jumuishi na maendeleo endelevu. Muhtsari huo umetaja changamoto za uwekezaji ikiwemo jinsi ya kuhakikisha mamlaka dhibiti ya nchi zinazopokea vitegauchumi zinaendelea kuwa fursa ya kufanya kazi yao na pia kushughulikia udhaifu wa kushughulikia migogoro kati ya mwekezaji na serikali. Kwa mantiki hiyo mwongozo huo wa UNCTAD unatoa mwarobani wa changamoto hizo ikiwemo wataalamu wa shirika hilo kusaidia kwenye utunzi wa sera za uwekezaji na kuwepo kwa mashauriano ya wazi yanayojumuisha wadau wote wakiwemo wasomi, wananhchi na watunga sera.