Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkurugenzi wa UNESCO alaani mauaji ya mwandishi wa Misri Ahmed Assem-el-Senousy

Mkurugenzi wa UNESCO alaani mauaji ya mwandishi wa Misri Ahmed Assem-el-Senousy

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO Irina Bokova, Jumatano amelaani vikali mauaji ya mwandishi mpiga picha wa magazeti nchini Misri, Ahmed Assem El-Senousy, na kuutaka uongozi wa nchi hiyo kuheshimu haki za waandishi habari, ili waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo na kwa mazingira ya usalama. Bi Bokova amezitaka pande zote nchini humo kutambua umuhimu wa kazi za waandishi habari na mchango wao. Amesema jamii kwa ujumla inategemea vyombo vya habari ambavyo viko huru na vinavyojitegemea ili kupashwa habari. El-Senousy, mwenye umri wa miaka 26 alikuwa mpiga picha wa gazeti la Al-Horreya-Wal-Adalah (Uhuru na haki) na alipigwa risasi na kuuawa Julai 8 alipokuwa akiripoti kuhusu maandamano.