Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban amteua abdoulaye Mar Dieye wa Senegal kuwa mkuu wa UNDP Afrika

Ban amteua abdoulaye Mar Dieye wa Senegal kuwa mkuu wa UNDP Afrika

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amemteua Bwana Abdoulaye Mar Dieye wa Senegal kuwa Msimamizi Msaidizi na Mkurugenzi Mkuu wa ofisi ya Afrika ya Mpango wa Maendeleo katika Umoja wa Mataifa, UNDP.

Bwana Dieye atamrithi Bwana Tegegnework Gettu, ambaye amechukua wadhfa mpya wa Naibu wa Katibu Mkuu wa masuala ya Baraza Kuu na usimamizi wa mikutano. Bwana Ban ameelezea shukran zake kwa Bwana Gettu kwa ukakamavu na kujitolea kwake kwa ajili ya Umoja wa Mataifa wakati alipokuwa akihudumu kama msaidizi wake na mkurugenzi mkuu wa UNDP barani Afrika.

Bwana Dieye ana uzoefu wa miaka mingi ya kuhudumu katika UNDP, ambako amefanya kazi hivi karibuni zaidi kama msimamizi wa wafanyakazi na mkurugenzi wa ofisi kuu ya UNDP tangu mwaka 2009.

Kabla ya wadhfa huo, aliwahi kuhudumu kama Naibu Msimamizi Msaidizi na Naibu Mkurugenzi wa kikanda wa UNDP katika ukanda wa nchi za Kiarabu, ambako alisimamia shughuli za shirika hilo Afrika Kaskazini, Mashariki ya Kati na mataifa ya ghuba ya Arabia. Bwana Dieye pia amewahi kushikilia nyadhfa nyingine za ngazi ya juu, zikiwemo za Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa operesheni za Umoja wa Mataifa nchini Cote d’Ivoire na nyinginezo katika ofisi ya UNDP barani Afrika.