Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhamiaji una faida na changamoto ambazo tunapaswa kukabiliana nazo: Vuk

Uhamiaji una faida na changamoto ambazo tunapaswa kukabiliana nazo: Vuk

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Vuk Jeremic, amesema uhamiaji ni suala la kuwepo daima katika historia ya mwanadamu, na hivyo kuzitaka nchi wanachama kujumuisha suala la uhamiaji katika mijadala yao kuhusu jinsi ya kupunguza pengo la kitofauti baina ya nchi tajiri na nchi maskini.

Bwana Jeremic amesema kwa miaka mingi, watu wamekuwa wakiacha mazingira na nchi zao za kuzaliwa na kuhamia mazingira na nchi za kigeni ili kutafuta maisha bora. Hata hivyo, amesema, licha ya faida zitokanazo na uhamiaji huu, kama vile kuchangia uchumi na hali ya maisha ya jamii zao na nchi wanakotoka, kuna utata wa kijamii inayozuka kutokana na uhamiaji.

Bwana Jeremic amesema katika mwongo mmoja uliopita, idadi ya wahamiaji wa kimataifa imeongezeka kutoka milioni 150 hadi milioni 214, na hivyo kufungua nafasi na changamoto nyingi kwa jamii kote duniani.

"Suala la uhamiaji limezua mijadala mikali kwani, licha ya uzuri unaotokana nao, uhamiaji huzua hisia tatanishi kijamii. Mijadala ya hivi karibuni kuhusu jinsi ya kuwajumuisha wageni katika baadhi ya nchi wanachama imekuwa ya kuzua utata. Wahamiaji wengi ni wahanga wa dhuluma na unyanyasaji unaotekelezwa na walanguzi na wasafirishaji haramu. Wengine hujikuta wamebanwa kwenye kuta za kutengwa na ubaguzi wa rangi au kikabila, pamoja na mazingira duni ya ajira, afya na makazi."