Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yatoa msaada wa dharura kwa raia wa DRC 66,000 walokimbilia Uganda

UNHCR yatoa msaada wa dharura kwa raia wa DRC 66,000 walokimbilia Uganda

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, UNHCR, linatoa msaada wa dharura unaojumuisha makazi, blanketi na vifaa vingine muhimu kwa wakimbizi wa DRC wapatao 66,00, ambao wamekimbilia Uganda kufuatia kuzuka mapigano siku tano zilizopita.

Watu hao walianza kukimbia kufuatia kundi la waasi la ADF kutoka Uganda kuuvamia mji wa Kamango ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, DRC.

Kundi hilo la waasi linasemekana kuendesha shughuli zake karibu na mlima Ruwenzori, kwenye mkoa wa Kivu ya Kaskazini. Kufikia Jumapili mchana, shirika la msalaba mwekundu nchini Uganda lilikuwa limeandikisha wakimbizi 66,139, ambao sasa wapo kwenye wilaya ya Bundibugyo magharibi mwa Uganda. Wakimbizi wanaowasili wanapokelewa kwenye shule tano za msingi na vituo vingine, huku wengine wakiishi na familia za watu binafsi.

Huku ikibainika kuwa hakuna dalili za wakimbizi hao kurudi nyumbani hivi karibuni, UNHCR iliungana na ofisi ya Waziri Mkuu nchini Uganda na mashirika mengine kuwapa msaada wa dharura. UNHCR pia inawahamishia wakimbizi kwenye kituo kipya cha muda, ambacho kipo takriban kilomita 23 kutoka mpakani na DRC.