Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani saba wa Kitanzania wa UNAMID wauawa na wengine 17 wajeruhiwaDarfur:

Walinda amani saba wa Kitanzania wa UNAMID wauawa na wengine 17 wajeruhiwaDarfur:

Walinda amani saba wa Kitanzania wa mpango wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wa kulinda amani Darfur UNAMID wameuawa na mtu asiyejulikana katika puruikshani mjini Darfur, Sudan, kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

Katibu Mkuu ameghadhabishwa baada ya kupokea taarifa ya shambulio hilo lililotokea Jumamosi asubuhi ya tarehe 13 Julai. Taarifa inasema mtu asiyejulikana alishambulia msafara uliokuwa na wanajeshi na polisi wa UNAMID kwenye eneo la Khor Abeche, Kusini mwa Darfur.

Mbali ya walianda amani hao saba waliokufa wengine 17 wamejeruhiwa miongoni mwao ni maafisa wa polisi wa UNAMID wakiwemo wanawake wawili na wanajeshi 13.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya walinda amani waliouawa, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wafanyakazi wote wa UNAMID.

Katibu Mkuu amelaani vikali shambulio hilo dhidi ya UNAMID, ambalo ni la tatu katika muda wa wiki tatu na anatarajia serikali ya Sudan itachukua hatua zinazostahili kuwafikisha wahusika kwenye mkono wa sheria.