Siku ya Malala ni siku ya kila mmoja ambaye amepaazia sauti haki zake:Malala

12 Julai 2013

Leo imetangazwa rasmi kuwa Siku ya Malala Duniani, na hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, kumefanyika hafla maalum, ambako amekaribishwa na kuongea mtoto wa Kipakistani, Malala Yousafzai, ambaye alinusurika kifo baada ya kushambuliwa na wanamgambo wa kitaliban mnamo Oktoba 9, mwaka 2012, wakipinga msimamo wake wa kutetea haki ya elimu ya watoto wasichana kwenye bonde la Swat, Pakistan.Mtoto Malala ambaye alivalia jozi la aliyekuwa Waziri Mkuu wa 11 wa Pakistan na mwanaharakati wa haki za binadamu, marehemu Benazir Bhuto, ameongea kwa ujasiri mkubwa, akisema kuwa anazungumza kwa ajili ya haki ya kila mtoto kupata elimu.

 Malala:

"Mnamo tarehe 9 Oktoba mwaka 2012, Wataliban walinipiga risasi upande wa kushoto wa uso wangu. Waliwalenga rafiki zangu pia. Walidhani kuwa risasi zingetunyamazisha. Lakini walishindwa. Na kutoka kwa kimya hicho, kuliibuka maelfu ya sauti. Magaidi walidhani kuwa wangebadili malengo yangu na kukomesha ndoto zangu, lakini hakuna kilichobadilika maishani mwangu: unyonge, uoga na kukosa matumaini vilikufa; nguvu, uwezo na ujasiri vilizaliwa”

 Malala pia ameusisimua ukumbi wa Baraza Kuu kwa moyo wake wa ukarimu na kuwatakia elimu hata watoto wa Wataliban

Malala

“ Wapendwa ndugu zangu na dada zangu, kumbukeni kitu kimoja: Siku ya Malala sio siku yangu. Leo ni siku ya kila mwanamke, kila mvulana na kila msichana ambaye amepaazia sauti haki zake. Simchukii mtu yeyote. Wala sipo hapa kuzungumzia ulipizaji kisasi dhidi ya Wataliban au kundi jingine lolote la kigaidi. Nipo hapa kuongea kuhusu haki ya elimu ya kila mtoto (applause). Nataka elimu kwa wavulana na binti za Wataliban na magaidi na wote wenye misimamo mikali.”