Baraza la Usalama laongeza muda wa ujumbe wa UNMISS

11 Julai 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limeptisha azimio la kuongeza muda wa kuhudumu kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS kwa kipindi cha mwaka mmoja, hadi Julai 15, 2014. Baraza hilo limesema hali nchini Sudan Kusini inatishia amani na usalama wa kimataifa katika ukanda mzima.

Baraza hilo pia limesema jukumu la kipaumbele kwa UNMISS ni kuhakikisha usalama wa raia, ikiwemo kuchukuwa hatua za dharura kuwalinda raia kutokana na hatari kwa maisha yao, bila kujali ni nani anayehatarisha maisha ya raia. Jukumu hilo linaambatana na lile la kuwezesha kuboreshwa kwa hali ya usalama, pamoja na kuwawezesha wenyeji kudhibiti mambo wenyewe. UNMISS inatakiwa pia kusaidia katika juhudi za kusuluhisha mizozo kwa njia ya amani.

Wanachama wa Baraza hilo pia wamelaani matukio ya machafuko ya mara kwa mara kwenye mpaka kati ya Sudan na Sudan Kusini, huku likizingatia hali tete iliyopo na ukosefu wa utulivu mpakani upande wa Sudan Kusini unaotokana na masuala ya mkataba mkuu wa amani ambayo hayajashughulikiwa.

Baraza hilo limeitaka serikali ya Sudan Kusini kuwajibika zaidi katika kuwalinda raia, na kuishauri ishirikiane zaidi na UNMISS. Pamoja na hayo, limezitaka pande zote kukomesha mara moja aina zote za ghasia na ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili dhidi ya raia wa Sudan Kusini, hususan ukatili wa kijinsia, ubakaji na aina zote za ukatili wa kingono na ukiukwaji wa haki za watoto.