Urusi yadai makundi ya upinzani Syria yalitumia silaha za kemikali

10 Julai 2013

Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa anaamini makundi ya upinzani yalojihami nchini Syria yametumia silaha za kemikali

Bwana Churkin amerejelea ripoti ya serikali ya Syria mapema mwaka huu iloyashutumu makundi ya upinzani kuwa yalirusha makombora yalojazwa gesi karibu na eneo la Khan al-Assal, kwenye jimbo la Aleppo.

Watu 26 waliripotiwa kuuawa na wengine 86 kujeruhiwa katika tukio hilo.

Serikali ya Syria iliomba msaada wa wataalam wa Urusi kuhakiki mambo, na ripoti ya wataalam hao ndio sasa imetolewa.

Balozi Churkin amesema ameiwakilisha ripoti hiyo kwa Katibu Mkuu mnamo siku ya Jumanne Julai 9, ikiwa ina ushahidi kuwa vikosi vya upinzani vilutmia gesi ya sarin.

Matokeo ya tathmini yanaonyesha wazi kuwa kile kilichotumiwa Khan al-Assal hakikuundwa viwandani, na kwamba kilijaa gesi ya sarin. Kwa hiyo, kuna kila sababu ya kuamini kuwa ni makundi ya upinzani yalojihami ndiyo yalotumia silaha za kemikali Khan al-Assal.”

Kufuatia ombi la serikali ya Syria, Katibu Mkuu Ban Ki-moon, alikuwa amemteua Profesa Ǻke Sellström wa Sweden kama mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuchunguza madai ya matumizi ya silaha za kemikali. Uchunguzi huo bado unaendelea.

Balozi Churkin amesema amekaribisha uamuzi wa serikali ya Syria kumwalika Bwana Sellström na mwakilishi mkuu wa masuala ya uondoaji silaha katika Umoja wa Mataifa, Bi Angela Kane kuzuru Syria.