UNCTAD yazindua ripoti ya uwekezaji huku nchi za Afrika zikifanya vizuri

10 Julai 2013

Shirika la Umoja wa Mataifa la biashara na viwanda UNCTAD, leo limetangaza ripoti ya hali ya uwekezaji ya dunia kwa mwaka 2013, huku nchi za Afrika zikichomoza kwa kuvutia wawekezaji wengi, wakati nchi zilizoendelea zikiendelea kujikongoja kutokana na athari ya mtikisiko wa uchumi wa mwakan2009.

Taarifa kamili na George Njogopa

Ripoti hiyo ambayo hutolewa kila mwaka ikiangazia hali jumla ya uchumi na biashara za kimataifa, inaonyesha kuwa bara la afrika ambalo linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa miundo mbinu ya kisasa limefaulu kusogea mbele ikilinganishwa na nchi zilizoko katika maeneo yaliyopiga hatua kimaendeleo.

Wakati mataifa yaliyoko dunia ya kwanza yakiendelea kuandamwa na jinamizi la kuporomoka kwa uchumi wa dunia uliojitokeza mwaka 2009, nchi za Afrika ambazo hazikuathirika moja kwa moja na hali hiyo zinapiga mwendo kusonga mbele.

Kulingana na ripoti hiyo, Afrika imefaulu kukuza kwa asilimia 5 kiwango cha uwekezaji wa kigeni, nah ii imechangiwa pia na kuendelea kupatikana kwa rasilimali ikiwemo sekta ya madini ambayo ambayo inakua kwa kasi.

Pamoja na mafanikio hayo, mkuu wa kitengo cha ushirikiano wa UNCTAD, Manuela Tortora amesema kuwa, Afrika bado inanafasi ya kufanya vizuri zaidi kama itaendelea kutoa msukumo wa jumuiya za kikanda kufanya kazi kwa umoja.

Cue

Utafiti wetu umebaini kuwa, iwapo nchi hizi zitatumia vyema mafungamano yao ya kikanda pamoja na jumuiya ndogo ndogo zilizopo, zinaweza kupiga hatua kubwa ikiwemo upanuaji wa wigo wa ajira na kutoa fursa ya kubadilishana teknolojia na kuendelea kuvutia zaidi uwekezaji wa kigeni.

Ripoti hiyo imeitaja Uganda kuwa ndiyo inayongoza katika eneo la Afrika Mashariki kwa kuwa na kiwango kikubwa zaidi cha uwekezaji wa kigeni, ikifuatiwa na Tanzania.

Akizungumza baada ya kuzinduliwa kwa ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Kituo cha uwekezaji Bi Juliet Kairuki alitaja kile alichokiita mageuzi yanayoendelea kutekelezwa na nchi maskini kuwa ndiyo chachu ya kuvutia wawekezaji wa kigeni.

Cue

Takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2012 Tanzania ilipata uwekezaji wa dola za marekani bilioni 1.7 tofauti na mwaka 2011 ambako uwekezaji ulikuwa ni bilioni 1.2