Mradi wa kuwashirikisha raia wa Sudan Kusini walio nje kwenye masuala ya afya wazinduliwa na IOM

9 Julai 2013

Huku taifa la Sudan likiadhimisha mwaka wa pili wa kuwa huru, Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM limezindua mpango wenye lengo la kuboresha huduma kwa wanadamu hususan zile za kiafya kwa kuwashirikisha wataalamu raia wa Sudan Kusini walio kwenye mataifa ya kigeni.Mradi huo unaofadhiliwa kwa kima cha dola 200,000 kutoka mfuko wa maendeleo wa IOM unalenga kuwatambua raia wa Sudan Kusini walio mataifa ya kigeni walio kwenye taaluma za afya na kutafuta njia za kuwashirikisha moja kwa moja au kupitia vyama ugenini.

Miaka mingi ya mizozo imesababisha kusambaratika kwa mifumo ya afya nchini Sudan Kusini ambapo chini ya asilimia 20 ya watu wote ndio hupata huduma za afya huku  kukiwa na daktari na wauguzi wawili kwa kila watu 100,000 kikiwa ni kiwango cha chini zaidi kuliko kilichoweka na shirika la afya duniani WHO cha wahudumu 250,000 kwa watu 100,000.