Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nafasi sawa na utajiri unaowanufaisha wote ni muhimu kwa maendeleo endelevu: Ban

Nafasi sawa na utajiri unaowanufaisha wote ni muhimu kwa maendeleo endelevu: Ban

Malengo ya maendeleo ya milenia yamepata ufanisi mkubwa katika kuchagiza hatua za kimataifa kuhusu masuala kadhaa, lakini, bado tofauti za kijamii na kiuchumi zinaendelea kukua katika nchi nyingi, ziwe maskini au tajiri, na hivyo kuweka doa la aibu kwa ahadi ya kimsingi ya mkataba mkuu wa Umoja wa Mataifa.Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Ban Ki-Moon, wakati akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambalo limekutana leo kujadili suala la kutokuwepo usawa wa kijamii na kiuchumi.

Bwana Ban amesema haki ya kijamii ni sehemu muhimu dunia yenye amani na endelevu kwa wanadamu wote. Katibu Mkuu amesema kuwa jamii ambazo matumaini na nafasi ni haba huwa katika hatari ya migogoro.

Tofauti za kijamii na kiuchumi huharibu utangamano wa kijamii na kuzuia mataifa kunawiri. Kutokuwa na usawa kunaweza kuibua uhalifu, magonjwa na uharibifu wa mazingira, na hivyo kuzuia ukuaji wa kiuchumi. Ikiwa mwanya wa tofauti utaendelea kupanuka, maendeleo hayawezi kuwa endelevu. Ndiyo maana usawa unaibuka kama nguzo muhimu katika mijadala ya ajenda ya maendeleo baada ya 2015.

Bwana Ban amesema kupunguza tofauti hizi kutahitaji mabadiliko ya kina na mikakati jumuishi ya maendeleo endelevu, pamoja na juhudi kubwa zaidi kutokomeza umaskini wa kupindukia na njaa.