Ni vyema Syria yataka kuzungumzia uchunguzi kuhusu silaha za kemikali: Ban

8 Julai 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amekaribisha kutaka kwa serikali ya Syria kuendelea na mazungumzo kuhusu ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuchunguza madai ya matumizi ya silaha za kemikali nchini humo.Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na msemaji wake, Bwana Ban ameelezewa kusikitishwa sana na madai hayo ya matumizi ya silaha za kemikali.

Mkuu wa ujumbe wa kuchunguza madai hayo, Dr. Åke Sellström, atasafiri kuja mjini New York wiki hii, ili kumpa Katibu Mkuu maelezo kuhusu shughuli zake. Ujumbe huo unaendelea kufuatilia hali ilivyo na kukusanya na kutathmini maelezo kutoka kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, wakati ukisubiri kupata idhini ya kwenda kwenye maeneo yalodaiwa kuathiriwa na matumizi ya silaha za kemikali.

Katibu Mkuu anatumai kuwa Syria itatoa idhini kwa ujumbe wa Bwana Sellström, ili ufanye uchunguzi wa kina kwenye maeneo kamili, huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa Syria ni muhimu kwa ujumbe huo kuweza kufanya uchunguzi wake kwa njia ya kuaminika.