Mkuu wa UNSOM alaani mauaji ya mwandishi Gaalkacyo:

8 Julai 2013

Mwakilishi maalumu wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Nicholas Kay, amebaini kwa masikitiko makubwa mauaji ya Libaan Abdullahi Farah ‘Qaran’ ripota wa Kisomali wa Kalsan TV iliyoko mjini Gaalkacyo.Ripoti zinasema Libaan alipigwa risasi na kuuawa Jumapili usiki akirejea nyumbani kutoka kazini. Bwana Kay amesema huyu ni mwandishi wa tano kuuawa kwa mwaka huu wa 2013 na hivyo kuifanyaSomaliakuendelea kuwa moja ya maeneo hatari sana kufanya kazi ya uandishi habari duniani.

Ameongeza kuwa hali ya kisiasa Puntland bado ni ya vuta nikuvute wakati wakijiandaa na uchaguzi na amewataka pande zote za kisiasa kujizuia na hali yoyote ya machafuko. Na amesisitiza umuhimu wa kuwalinda waandishi habari na kutetea uhuru wa vyombo vya habari.

 Bwana Kay ametuma salamu za rambirambi kwa familia na marafiki wa ibaan Qaran na waandishi na vyombo vyote vya habari nchini Somalia akiwahakikishia kwamba mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNSOM umejidhatiti kufanya kazi na serikali ya Somalia kuimarisha usalama na sekta ya haki na sheria ili kuhakikisha kwamba Somalia iko salama na wachochezo wowote wa ghasia na uhalifu wanafikishwa kwenye mkono wa sheria.