Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marekani, Switzerland zaipiga jeki IOM kuwanuru raia wa DRC

Marekani, Switzerland zaipiga jeki IOM kuwanuru raia wa DRC

Juhudi zinazoendeshwa na shirika la kimataifa linalohusika na uhamiaji IOM, kwa raia wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo waliokosa makazi, zimepata msukumo mpya kufuatia mchango wa kiasi cha dola za Marekani milioni 3 ambazo zinatazamiwa kutumika kwa ajili ya kuendesha tathmini kwa ajili ya raia hao waliokosa makazi.

Kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na serikali ya Marekani kupitia mfuko wake wa usaidizi wa majanga kinaongeza uhai mkubwa kwa IOM ambayo pia imepokea kiasi kingine cha fedha dola 670,000 kutoka shirika la maendeleo la Uswis.

Hali jumla katika eneo la Mashariki mwa Congo imeendelea kusalia tete kufuatia mfululizo wa mapigano yaliyozuka katika kipindi cha mwezi May mwaka huu baaina ya vikosi vya serikali na waasi wa kundi la M23 .

Mafungu hayo ya fedha yataiwezesha IOM kuendesha shughuli za kuwatambua raia waliokosa makazi ikiwemo pia kukusanya taarifa mbalimbali kuhusiana mwenendo jumla wa eneo hilo.