FAO, WFP waonya kuhusu hali mbaya ya chakula Syria

5 Julai 2013

Ripoti moja iliyotolewa na mashirika ya Umoja wa Mataifa inasema hali ya upatikanaji chakula nchini Syria ni mbaya na kwamba kunauwezekano mkubwa wa kuanguka kwa shughuli za kilimo katika kipindi cha miezi 12 ijayo.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa kwa pamoja baina ya Shirika la chakula la kilimo FAO na lile la mpango wa chakula duniani WFP, imetaja sababu ya kuanguka kwa shughuli za uzalishaji wa kilimo ni matokeo ya mapigamo yanayoendela sasa.

Imesema hali ya uzalishaji mazao pamoja na shughuli za ufugaji siyo ya kuridhisha na kwamba tatizo hilo linaweza kuwa baya zaidi katika kipindi cha mwaka ujao iwapo mapigano hayo yataendelea.

Ripoti hiyo inafuatia tathmini iliyofanywa na wataalamu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa waliotembelea Syria katika kipindi cha mwezi May na Juni mwaka huu.

Mashirika haya ya Umoja wa Mataifa yanasema kuwa Syria inahitaji kuagiza kiasi cha tani milioni 1.5 za ngano katika kipindi cha sasa hadi mwakani.Hali ya uzalishaji wa ngano inakadiriwa kufikia tani milioni 4 kw wakati huu, kiwango ambacho kimeanguka kwa asilimia 15 kulikosababishwa na mapigano hayo.