Muafaka wafikiwa kuongeza idadi ya kutembelea familia za Sahrawi zilizotengana:

3 Julai 2013

Mkutano uliofanyika Geneva baiana ya serikali ya Morocco, Frente Polisario, Algeria, Mauritania na shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, umemalizika leo kwa makubaliano ya kuongeza mpango wa familia kutembelea jamii zao baiana ya wakimbizi wa Sahara Magharibi wanaoishi kwenye kambi karibu na Tindouf, Algeria, na familia zao zilizopo kwenye himaya ya Sahara Magharibi.

Rukhsa hiyo ya kumbeleana ni kipengee muhimu katika mpango wa UNHCR wa kujenga kujiamini na imani, hatua zilizokuwa zikiendelea tangu mwaka 2004 kwa lengo la kusaidia familia za Sahrawi zilizotengana kwa zaidi ya miaka 37 katika moja yahali ya ukimbizi wa muda mrefu sana duniani.

Kitu kingine muhimu katika mpango wa UNHCR ni kujenga imani na uaminifu ili kusaidia juhudi za Umoja wa Mataifa za kutafuta suluhu ya kisiasa ya mgogoro wa Sahara Magharibi.

Washiriki wa mkutano wamesema kwamba chaguo la kurejea kwa hiyari katika makazi yao ya asili itakuwa muhimu kwa suluhisho lolote la kisiasa siku za usoni chini ya ushawishi wa Umoja wa mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon pia ametuma ujumbe wa kutia moyo na kuunga mkono akiwachagiza washiriki kutafuta njia muafaka ya kupanua wigo wa mpango wa kujenga hali ya kujiamini kwa watu hao.