Uhamishiaji wa teknoljia Afrika waangaziwa katika mkutano wa ECOSOC

3 Julai 2013

Mkutano wa Baraza la masuala ya kiuchumi na kijamii katika Umoja wa Mataifa, ECOSOC unaendelea mjini Geneva, Uswisi, ambapo mada kuu ya majadiliano hii leo imekuwa ni ushirikiano wa kimataifa katika kuendeleza, kuhamishia na kupanua matumizi ya teknolojia barani Afrika. Joseph Msami na taarifa kamili(TAARIFA YA JOSEPH MSAMI)

Kikao hicho kuhusu utekelezaji kimesikiliza taarifa za mikakati ya kusaidia kuendeleza dhima kuu ya mkutano wa kila mwaka wa mawaziri kuhusu sayansi, teknolojia, ubunifu, na mchango wa utamaduni katika kuendeleza maendeleo endelevu na kufikia malengo ya maendeleo ya milenia, MDGs.

Akizungumza katika kikao hicho, rais wa Colombia, Juan Manuel Santos amesema changamoto zinazomkumba mwanadamu sasa zimekuwa kanganyishi hata zaidi, lakini kuna pia fursa nyingi za kudakia ili kufanya maendeleo katika haki, usawa na uendelevu.

Amesema kuleta maendeleo endelevu na kutokomeza ufukara ni changamoto zinazokwenda sambamba, na ambazo zinahitaji hatua za kina kutoka kwa serikali, wanazuoni na mashirika ya umma.

Ameongeza kuwa utekelezaji haupo katika ngazi zote, na kwamba matokeo yalotarajiwa hayajafikiwa, na kwa hiyo, juhudi zaidi zahitajika.