Watoto ndio wanaoathirika zaidi na hali kuzorota CAR: UNICEF

2 Julai 2013

Hali ya kibinadamu kwa watoto katika Jamhuri ya Afrika ya Kati imezidi kuwa mbaya tangu serikali ya kijeshi kuingia mamlakani nchini humo, kwa mujibu wa tathmini zilizofanywa na Shirika la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa Mataifa, UNICEF.Tathmini hizo zinaonyesha kuwa watoto kati na magharibi mwa nchi hiyo ndio waloathirika zaidi. Utoaji wa huduma za afya umeathirika zaidi, huku dawa zikipatikana tu katika nusu ya vituo vya afya na hospitali katika maeneo hayo.

UNICEF pia inasema ni watoto watatu tu kati ya watoto kumi ndio wanaokwenda shule. Tathmini hizo zinaonyesha kuwa familia nane kati ya kumi zimelazimika kubadili mlo kwa kiasi kikubwa, kwani aina nyingi za vyakula vya kutegemewa havipo.

Msemaji wa UNICEF, Marixie Mercado, amesema kuna haja ya kupeleka misaada ya dharura kule ambako inahitajika zaidii.

“Hata kabla ya wanajeshi kunyakuwa mamlaka, Jamhuri ya Afrika ya Kati tayari ilikuwa mojawapo ya mahali pagumu zaidi kwa mtoto kuishi, ikijikuta katika nchi kumi za mwisho mara kwa mara kwa mujibu wa viashiria vya maendeleo. Tathmini zinaonyesha kuwa mahitaji yameongezeka na kupanuka, na kwamba watoto ndio wanaoathiriwa zaidi na umaskini wa kupindukia, uongozi mbaya, mizozo na kutokuwepo utulivu wa kisiasa.”

Kumekuwa na ongezeko kubwa la visa vinavyoripotiwa vya dhuluma za nyumbani, watoto walio pweke na watoto kuingizwa katika makundi ya silaha.

UNICEF inasema yapata watu 206,000 wamelazimika kuhama makwao, 50,000 wametafuta hifadhi katika nchi jirani, wengi wao wakiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.