Hatua zilizopigwa Afghanistan zapaswa kutunzwa: Jan Eliasson

2 Julai 2013

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Yan Eliasson, ambaye yuko ziarani nchini Afghanistan, amesema nchi hiyo imepiga hatua za kuridhisha katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita, na ambazo zinapaswa kutunzwa. Joshua Mmali ana taarifa kamili

(TAARIFA YA JOSHUA MMALI)

Bwana Eliasson ambaye ameuzuru mji mkuu wa Kabul na kutembelea jimbo la Kandahar, amewaambia waandishi wa habari kuwa taifa la Afghanistan limepiga hatua muhimu katika katika kujenga taasisi za taifa la kidemokrasia, kuendeleza afya na elimu, haki za binadamu, hususan hatua kubwa zilizopigwa katika kuendeleza haki za wanawake.

Bwana Eliasson amesema taifahilosasa limeingia katika kipindi kipya katika masuala ya usalama, maendeleo na jamii kwa ujumla.

Naibu huyo wa katibu mkuu amesema kuna haja ya kuhakikisha kuwa hatua hizi za ufanisi zilizopigwa zinatunzwa, ili watu waAfghanistanwaendelee zaidi katika kuweka amani,  na kuahidi uwepo wa Umoja wa MataifaAfghanistan, licha ya lolote lifanyikalo baada ya mwaka 2014.

“Tunafahamu kuwa tuna jukumu muhimu hapa kwa namna nyingi, na tu tayari kutimiza jukumu hilo, tukishirikiana na serikali ya Afghanistan, taasisi, na watu wa Afghanistan. Hakuna njia nyingine ya kuweka mabadiliko ya kidemokrasia, utulivu na maendeleo, bali katika uchaguzi wa wazi, jumuishi na wa kuaminika, kama ulivyowekwa katika katiba ya Afghanistan. Hiyo pia ndiyo njia moja muhimu ya kutunza mafanikio mliyoyafikia katika miaka kumi na miwili ilopita."