Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya ujumbe wa MINUSMA yafunguliwa rasmi nchini Mali

Ofisi ya ujumbe wa MINUSMA yafunguliwa rasmi nchini Mali

Hafla ya kuhamishwa kwa mamlaka kutoka kwa vikosi vya kimataifa vya kusaidia nchi ya Mali chini ya Uongozi wa Waafrika, (MISMA) hadi kwa ujumbe mpya wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini humo, MINUSMA, imefanyika leo mjini Bamako, na hivyo kuanza rasmi operesheni za walinda amani nchini Mali. Joshua Mmali na taarifa kamili

(TAARIFA YA JOSHUA)

Hafla hiyo ya kufungua rasmi ofisi za MINUSMA ambayo imeongozwa na waziri wa ulinzi wa Mali, Jenerali Yamoussa Camara, imehudhuriwa pia na Mwakilishi maalum wa Muungano wa Nchi za Afrika, Pierre Buyoya na Mkuu wa masuala ya ulinzi wa amani katika Umoja wa Mataifa, Hervé Ladsous, na Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu nchini Mali, Bert Koenders, ambaye pia ni mkuu wa MINUSMA

Akiongea wakati wa hafla hiyo, Bwana Koenders amesema kuanzishwa kwa ofisi ya MINUSMA kumetokana na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo limesisitiza ahadi ya jamii ya kimataifa kuwasaidia wananchi wa Mali katika kutafuta utulivu, amani na maendeleo.

Akiongea mjini Geneva wakati wa kufungua mkutano wa ECOSOC, Katibu Mkuu wa Unmoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, amesema anatiwa wasiwasi na hali ya kibinadamu nchini Mali, ambako takriban watu laki nne sabini na tano elfu wamelazimika kuhama makwao, huku wengine milioni 1.4 wakihitaji misaada ya dharura.