Mienendo ya idadi ya watu ni fursa nzuri kwa bara Ulaya , Marekani na Asia :UM

1 Julai 2013

Hali ya sasa ya mienendo ya idadi ya watu barani Ulaya, Marekani na Asia ya Kati ni kama fursa na wala si tisho kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiwemo lile la mfuko wa idadi ya watu na tume ya uchumi ya Umoja wa Mataifa kuhusu uchumi barani Ulaya UNECE kwenye mkutano uliong’oa nanga hii leo mjini Geneva. Maafisa hao wanasema kuwa kadri miaka inavyokwenda maeneo hayo yanastahili kuwekeza zaidi kwenye sekta za elimu, afya na ajira. Wanasema kuwa mienendo ya sasa ya idadi ya watu ndiyo nguzo muhimu kwenye maendleo na fusra nzuri kwa vizazi vinavyokuja. Utafiti unaonyesha kuwa watu katika maeneo hayo wanaishi maisha marefu, yenye afya na wana viwango vya juu vya masomo kuliko vizazi vilivyopita.

Kulingana na takwimu mpya zitakazowasilishwa mbele ya mkutano huo ni kwamba idadi yote ya watu katika eneo hilo ilifikia watu bilioni 1.24 mwaka 2010. Kutokana na watu kuishi miaka mingi na idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa watu wanazidi kuzeeka huku idadi ya watu walio na zaidi ya miaka 65 na kuendelea ikoongezeka kwa asilimia 14 au watu milioni 174.5.