Mfumo mpya waanzishwa kuwezesha nchi kupata takwimu sahihi za misitu: FAO

28 Juni 2013

Shirika la kilimo na chakula duniani, FAO limeanzisha mfumo mpya kwenye mtandao ambamo kwao nchi wanachama zitaweza kutumia kuboresha tathmini zao za ukubwa wa misitu, ujazo wa miti na uwezo wa miti kwenye misitu hiyo kuvuta hewa ya ukaa, kama njia mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.FAO inasema kuwa kwa kufanya hivyo nchi zitaweza kukuza misitu yao kwa kupanda miti na hata kuendeleza matumizi ya nishati mbadala. Kupitia mfumo huo watafiti, wanasayansi na maafisa misitu watawaweza kukokotoa ujazo wa misitu na hata hewa ya ukaa iliyovutwa na miti hiyo na hivyo kusaidia watunga sera kufanya maamuzi sahihi ya mikakati ya kukabiliana na tabianchi.

Hii ni mara ya kwanza kwa nchi kuweza kuingia katika mfumo huo wa takwimu za aina ya miti inayotumika kutathmini rasilimali za misitu duniani kote, amesema Matieu Henry Afisa Misitu wa FAO akiongeza kuwa watafiti watatumia mfumo huo kupima kipenyo na urefu wa mti na uzito wa mti mzima iwapo utapondwa pondwa. Kwa upande wa Afrika, mfumo huo una aina 324 za miti kutoka kanda Tisa tofauti za ekolojia.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud