Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laondoa vikwazo dhidi ya Iraq, laongeza muda wa UNDOF

Baraza la Usalama laondoa vikwazo dhidi ya Iraq, laongeza muda wa UNDOF

Baraza la Usalama leo kwa kauli moja limepitisha azimio la kuiondolea nchi ya Iraq vikwazo vyote ilivyowekewa kutokana na uvamizi wake kwa taifa la Kuwait mwaka wa 1990 na madai ya kuwa na silaha za nyuklia na za kemikali. Vikwazo dhidi ya Iraq viliwekwa mnamo mwaka 1991, wakati wa uongozi wa Saddam Hussein.

Baraza hilo pia limemwomba mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuisadia Iraq kuendeleza, kusaidia na kuwezesha juhudi za kurejesha raia wa Kuwait na wan chi nyingine, na mali ya Kuwait iloporwa na Iraq.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kura ya Baraza la Usalama, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Bwana Hoshyar Zebari, amesema leo ni siku mpya katika historia ya nchi yake, na sasa wataangazia ukurasa mpya wa uhusiano kati ya Iraq na Kuwait sasa na siku zijazo.

"Vikwazo dhidi ya Iraq vimekuwa kitu cha kale sasa. Tunahisi nchi zote mbili zimeshirikiana vyema, na tumweweza kufunga daftari zote zilizokuwa zimesalia chini ya aya ya saba ya Mkataba Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Huu ni mwanzo mpya wa uhusiano kati ya nchi zetu jirani na ndugu. Tumefurahishwa na kura ya kauli moja ya Baraza la Usalama kwa hili. Huu ni mfano kwa nchi nyingine pia kutatua mizozo yao kwa njia ya amani."

Katika hatua nyingine, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuongeza muda wa kuhudumu kwa ujumbe wake wa uangalizi wa makubaliano ya usitishaji uhasama baina ya Israel na Syria, UNDOF katika eneo la Golan kwa muda wa miezi mingine sita, hadi mwishoni mwa mwaka huu 2013.