Tuwezeshe ujasiriamali kwa vijana ili kubuni nafasi za kazi: Ban

26 Juni 2013

Wakati vijana zaidi ya milioni 70 wakiwa hawana ajira, ujasiriamali unaweza kuwa suluhu la kuwabadilisha vijana hao wasio na ajira na kuwafanya kuwa watoaji ajira wakubwa. Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja huo wakati likukutana kujadili ujasiriamali kwa maendeleo.

Bwana Ban amesema kati ya miaka 2016 na 2030, takriban vijana milioni 425 watahitaji ajira.

Ameongeza kuwa ili kusaidia kukabiliana na changamoto hii, viongozi wanatakiwa kuwatia moyo, kuwaelimisha na kuwapa uwezo vijana wajasiriamali.

Vijana wengi sana wanajikuta wamenaswa katika mizozo na kuishi katika umaskini au kuhangaika hata kupata chakula tu. Tunatakiwa kuwapa mazingira salama na ya amani ili waweze kukuza stadi zao na kutoa mchango kwa jamii zao. Tufanye kila tuwezalo kuwatunza vijana na kufungua matumaini yao ya siku zijazo.”

Bwana Ban amesema kuwa kutafuta masuluhu kwa changamoto za maendeleo endelevu ndiyo njia pekee ya kujenga siku zijazo tuzitakazo. Amesema masuluhu hayo yanapaswa kuwa yale yanayobuni nafasi za ajira na kuchagiza ukuaji.

Amesema ujasiriamali unahusu ubunifu, kuvunja vizuizi, ujasiri na kuonyesha kuwa mitindo mipya ya biashara inaweza kukabiliana na matatizo ya muda mrefu.