UNESCO yalaani mauaji ya mwandishi Uganda.

26 Juni 2013

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCO Irina Bukova ameitaka mamlaka nchini Uganda, kuendesha uchunguzi wa kina kuhusu mauaji ya mwandishi wa habari Thomas Pere ambaye mwili wake ulikutwa nje kidogo ya mji wa Kampla June 17 mwaka huu.

Katika taarifa yake aliyoitoa mjini Paris Ufaransa, Bi Bukova amesema analaani mauaji hayo na kutaka juhudi zifanywe ili kuweka nuruni kifo cha mwanahabari huyo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wahusika.

Bi Bukova pia amesema mauaji ya mwandishi wa habari ni uhalifu dhidi ya jamii nzima kwa ujumla huku akiita hatua hiyo ukandamizaji wa mjadala wa kidemokrasia na kunyamazisha haki ya msingi ya uhuru wa kujieleza.

Mkurgenzi huyo mkuu wa UNESCO amekwenda mbali zaidi na kusema ni lazima wafanyaji wa uhalifu huo wafikishiwe ujumbe kwamba matendo yao hayatanyamaziwa, yataadhibiwa.

Thomas Pere alikuwa mwandishi wa habari wa gazeti liitwalo New Vision na alikuwa akiripoti maswala ya kijamii. Thomas ambaye alikuwa mwanachama hai wa kundi la waandishi wasio na mipaka anakuwa mwandishi wa nne kuuwawa tangu September 2010 na kwa mara ya mwisho alionekana jioni ya June 16 akitoka ofisini kuelekea nyumbani kabla ya mwili wake kupatikana asubuhi siku iliyofuata.