Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili hali Mashariki ya Kati

Baraza la Usalama lajadili hali Mashariki ya Kati

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekutana na kushauriana kuhusu hali ya usalama Mashariki ya Kati, ukiwemo mizozo ya Syria, na suala la Palestina.

Katika mkutano huo, Naibu wa Mkuu wa masuala ya Kisiasa katika Umoja wa Mataifa, Fernandez Taranco, ameliambia Baraza la Usalama kuwa hali katika Mashariki ya Kati inaufanya sasa kuwa wakati mgumu kwa Umoja wa Mataifa, na uwezo wake wa pamoja wa kutimiza kanuni za Mkataba wake Mkuu umewekwa kwenye mtihani mgumu.

Hata hivyo, Bwana Taranco ambaye amezungumza kuhusu mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya jeshi la Lebanon, mgogoro wa Syria na suala la Palestina, amesema Baraza la Usalama na Umoja wa Mataifa hauwezi kufa moyo na kukubali hali ya kufeli kwa pamoja kufanya upuuze wajibu wake.

 “Kutatua mizozo na kutafuta njia ya kuishi pamoja kwa amani na kwa kuheshimiana kunawezekana. Lakini kunahitaji ujasiri na ulegezaji misimamo katika nyanja za kitaifa, kikanda na kimataifa, na kujitolea kutatua mizozo kwa njia ya amani, siyo kwa njia ya vita au ghasia. Haya ni kweli Syria na kwingineko. Ni muhimu kwa wote kuwajibika na kuchangia kugeuza hali inayochangia uhasama katika ukanda [wa Mashariki ya Kati].”

Akiongea na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Mwakilishi wa Kudumu wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa, Bashar Jaafari amesema kuwa timu ya wataalam wa Umoja wa Mataifa wanaotakiwa kuchunguza madai ya matumizi ya silaha za kemikali inakubaliwa kwenda Syria hata sasa, japo inapaswa kuzingatia tu maeneo ambayo serikali ya Syria imekubali timu hiyo kuzuru.