Ukiukwaji wa haki za binadamau bado tishio Sudan:UM

21 Juni 2013

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Sudan Mashood Baderin amesema licha ya hali ya haki za binadamu kuimaraika nchini humo , bado kuna changamoto ya ukiukwaji wa haki hizo katika baadhi ya sehemu.

Akitoa ripoti ya ziara yake ya tatu nchini humo, mtaalamu huyo amesema leo mjini Geneva kuwa jumuiya ya kimataifa inapaswa kuisaidia mamlaka ya Sudan misaada ya kiufundi pamoja na kujengea uwezo.

Mathalani Bwana Baderin akizungumzia hali ilivyo katika jimbo la Darfur, amesema ongezeko la migogoro na mapigano ya kikabila baina ya vikundi vyenye silaha na majeshi ya serikali yamesababisha kuzorota kwa amani na watu kupoteza makazi ambapo kwa mwezi na nusu takribani watu 4500 wameshuhudiwa wakipoteza makazi na hivyo kuwa wakimbizi wa ndani katika kambi iitwayo Otash jimboni humo ambapo wanaishi katika mazingira magumu hususani wanawake na watoto.

Amelaani ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo la Kordofan Kusini akitolea mfano wa makombora ya hivi karibuni katika mji wa Kadugli yaliyosababisha kifo cha mlinda amani na kuongeza kuwa mashambulizi yanayofanywa na waasi katika meneo kadhaa yanawaathiri raia wasio na hatia.

Bwana Baderin pia amekaribisha uzinduzi wa Mpango wa kitaifa wa haki za binadamu uliofanyika June 19 kwa kupongeza serikali ya Sudan kwa ahadi yake kutekeleza majukumu ya haki za binadamu kimataifa na kuwaachia baadhi ya viongozi wa upinzani waliokuwa wamewekwa kizuizini.

Ripoti ya mataalamu huyo huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu ataiwasilisha katika baraza la haki za binadamu mwezi September mwaka huu.