Waasi washambulia zaidi baada ya serikali kuchukua hatamu za ulinzi Afganistan: UM

20 Juni 2013

Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa nchini humo Jan Kubiš amesema kwa sasa kuna dalili dhahiri shahiri kwa Jumuiya ya kimataifa kuendeleza usaidizi wake kwa Afghanistan hadi mwakani na zaidi kwa njia ambazo zitaimarisha uongozi wa nchi hiyo.

(SAUTI YA Jan)

"Kama ilivyotangazwa wiki hii, majeshi ya Afghanistani yameingia awamu ya mwisho ya kushika hatamu za ulinzi nchini kote. Vikundi vinavyopinga serikali hata hivyo vinatafuta njia za kupingana na hali hiyo kwa kuwalenga raia na maafisa wa usalama huku wakitisha raia. Lengo lao ni kutikisa imani ya wananchi kwa serikali na jeshi lake la ulinzi.”

Bwana Kubiš ameenda mbali zaidi na kusema kuwa kuna ongezeko la mashambulio ya kikatili dhidi ya wanaounga mkono serikali, watumishi wa umma na wale wa mahakama, vitendo ambavyo ni kinyume na sheria za kimataifa na hata maadili ya vita.

Majeshi ya kimataifa yanayosaidia Afghanistan yanatarajiwa kujiondoa kabisa nchini humo mwishoni mwa mwaka ujao.