Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lashutumu shambulio Somalia, lasema ni la kigaidi

Baraza la usalama lashutumu shambulio Somalia, lasema ni la kigaidi

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshutumu shambulio la kigaidi lililotokea Jumatano asubuhi nchini Somalia ambalo tayari kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab kimedai kuhusika nalo.

Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Juni Balozi Lyall Grant, kutoka Uingereza amesema kwa pamoja wajumbe wamesifu kitendo cha ujasiri cha ujumbe wa umoja wa Afrika huko Somalia, AMISOM na jeshi la Somalia kwa hatua walizochukua punde baada ya shambulio hilo lililosababisha vifo na majeruhi kadhaa.

Amesema wajumbe wamesisitiza ugaidi wa aina yoyote ile na vitendo husika ni moja ya vitisho vikubwa vya amani na usalama duniani na kwamba vitendo vya aina hivyo haviwezi kuhalalishwa kwa misingi yoyote ile.

(SAUTI YA BALOZI)

Balozi Grant amesema kuwa Baraza la usalama limesisitiza kuwa ugaidi kamwe hautapunguza kasi ya usaidizi kwa Somalia katika kipindi hiki cha mpito na zaidi ya yote wajumbe wameelezea utayari wao wa kuchukua hatua dhidi ya wale wote wanaotishia amani, utulivu na usalama huko Somalia.