Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay aitaka Myanmar kukomesha vitendo vya kibaguzi

Pillay aitaka Myanmar kukomesha vitendo vya kibaguzi

Mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu Navi Pillay ameitolea mwito serikali ya Myanmar kuhakikisha kwamba inaendelea kupambana na vitendo vya ubaguzi vinavyojitokeza kwenye maeneo ya kikabila na imani ya kuabudu.

Pillay amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la ubaguzi kwa makundi machache ya watu ambao wanabaguliwa kutokana na makabila yao ama dini zao, akisema kuwa kushindwa kutafutia ufumbuzi kwa kasoro hizo, kunaweza kukwaza pia juhudi za kuleta mageuzwi zinazotekelezwa sasa.

Akielezea zaidil, Pillay amesema kuwa kuendelea kuwakandamiza jamii ya watu wa Rohingya waliko katika jimbo la Rakhine na kuenea kampeni ya kupiga marafuku imani Kiislamu kunatishia harakati za kuleta mageuzi na kusisitiza kuwa serikali inapaswa kuamka sasa.

Kiasi cha watu 140,000 wengi wao wakiwa wa jamii ya Rakhine wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na mapigano yaliyozuka katika miezi ya karibuni baina ya waumini wa Buddha na jamii ya Waislamu.