Baraza la Usalama lajadili hali nchini Libya

18 Juni 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kujadili hali nchini Libya. Joshua Mmali amekuwa akifuatilia mambo katika Baraza hilo.

 (TAARIFA YA JOSHUA MMALI)

 Changamoto za kisiasa na kiusalama zinazoikabili Libya sasa hivi huenda zikawa ni matokeo ya miongo ya uongozi wa kiimla, kutokuwepo taasisi imara za kitaifa, pamoja na hali kanganishi ya mienendo ya kisiasa. Hayo yamesemwa na Bwana Tarek Mitri, ambaye ni Mwakilishi Maalum wa katibu Mkuu kuhusu Libya na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuisaidia Libya, UNSMIL.

Bwana Mitri amesema kuwa hali hii inahitaji mdahalo wa kitaifa wa kisiasa, ambao utatoa makubaliano kuhusu masuala ya kipaumbele katika kipindi cha mpito.

 Huu ndio ujumbe ambao nimekuwa nikitoa kwa mamlaka za Libya za ngazi za juu zaidi, viongozi wa kisiasa na wa mapinduzi. UNSMIL tayari imetoa ushauri kwa serikali pamoja na Bunge Kuu la Kitaifa kuhusu jinsi ya kuendesha mdahalo wa kitaifa. Tu tayari kusaidia harakati hizo, ikiwa tutaombwa na mamlaka za Libya.

 Pamoja na hayo, Bwana Mitri amelifahamisha Baraza la Usalama kuhusu mfumo mzima wa sheria nchini Libya, vikiwemo vifungo vinavyokiuka sheria, hali ya wafungwa nchini Libya, na mauaji ya kiholela. Amesema pia kuwa UNSMIL inaendelea kusikitishwa na hali ya wahamiaji na wakimbizi wa ndani nchini Libya, ambayo ni mbovu mno.