Baraza la Usalama lamulika hali ya watoto katika vita vya silaha

17 Juni 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limefanya kikao kuhusu hali ya watoto katika vita vya silaha, ambapo pia limepokea ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu watoto katika katika vita, ambayo imesema hali ilikuwa mbovu hata zaidi katika kipindi cha miezi 18 ilopita, wakati mizozo mipya ilipoibuka au ile iliyopo kuenea zaidi.

Akiongea wakati wa kikao hicho, Mwakilishi wa Katibu Mkuu kuhusu watoto na vita vya silaha, Leila Zerrougui, amesema wahusika wasio wa kiserikali katika mizozo wanachangia kwa kiasi kikubwa zaidi ukiukwaji wa haki za watoto.

“Kama katika miaka iliyopita, wahusika wasio wa kiserikali ndio wengi zaidi kwenye orodha hii. Wao ni arobaini na sita, kati ya jumla ya wakiukaji 55 walioorodheshwa katika ripoti hii. Kuna sababu mpya za kuhofia watoto, ambazo zitakaiwa kukabiliana nazo haraka, zikiwemo matumizi ya shule na wanajeshi, kuwazuilia watoto wanaodaiwa kuhusika na makundi yenye silaha na athari za matumizi ya ndege za vita zisizo na rubani kwa watoto.”

Miongoni mwa nchi ambako haki za watoto zimetajwa kukiukwa katika ripoti hiyo ni Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Syria, huku Chad na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zikisifiwa kwa hatua zilizopiga kwa kuonyesha hamu ya kuzingatia maazimio ya Baraza la Usalama, na kuweka sheria za kuwalinda watoto katika mizozo.

Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa Mataifa, Yoka Brandt, amesema lililo muhimu zaidi katika kukomesha ukiukwaji wa haki za watoto katika vita, ni pande zinazozozana kuwajibika kulinda haki za watoto, na wale wanaozikiuka kukabiliwa na mkono wa sheria.

“Tunatoa wito kwa pande zinazozozana kubuni mbinu mpya katika mapigano. Tunawasihi wasiviweke vikosi vyao katika maeneo ya raia, wala kushamuliana katikati mwa vijiji na miji. Pili, ni matumizi ya shule katika operesheni za kijeshi. UNICEF inasikitishwa sana na hali hii. Inawaweka watoto na walimu hatarini, inawapora watoto fursa ya kusoma, na kukiuka haki yao ya elimu.”