UM wakaribisha fursa mpya kwa wakimbizi wa ndani Georgia

17 Juni 2013

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu kwa wakimbizi wa ndani, Chaloka Beyani ametaka Georgia kutumia mwelekeo jumuishi katika kushughulikia masuala ya wakimbizi wa ndani ikiwemo wale wa miaka ya 1990 na 2008 pamoja na wale ambao wamepoteza makazi kutokana na majanga ya kiasili. Kauli hiyo ameitoa mwishoni mwa ziara yake ya siku tano nchini humo kama anavyoripoti George Njogopa.

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Mtaalamu Beyani ameipongeza serikali yaGeorgia kutokana na hatua yake kumwalika nchini humo ambako alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali na kujionea namna serikali hiyo inavyochukua hatua ya kuboresha maisha kwa ajili ya wakimbizi wa ndani. Alikuwa nchini humo kuanzia Juni 10 hadi 14 ambako pia alitoa mwito akitaka kuchukuliwa hatua za kuboresha ustawi na maisha jumla ya watu waliokosa makazi kutokana na machafuko yaliyotokea mwaka 2008.

Georgia imekuwa ikitajwa kuwa ni miongoni mwa nchi za kupigiwa mfano, iliyoweza kuboresha ustawi jumla wa watu wake waliokosa makazi kwa kuazisha miradi ya ujenzi wa nyumba na kusambaza mahitaji mengine muhimu ili kuwakirimu wananchi walioathiriwa na mapigano hayo ya mwala 2008. Akirejelea ziara iliyoifanya mtangulizi wake, Walter Kaelin,Bwana Beyani alisema kuwa pamoja na utashi unaonyeshwa na serikali ya Georgia, lakini hata hivyo alisema kuwa, bado nchi hiyo inakabiliwa na mikwamo ya kisiasa ambayo imefanya baadhi ya raia waliokwenda nchi za nje kushindwa kurejea nyumbani. Amezitaka mamlaka husika kuzifanyia kazi changamoto za kisiasa zilizosalia ili kupatikane maridhiano ya kudumu.