Côte d’Ivoire mwelekeo ni mzuri lakini bado kuna mparaganyiko: Mtaalamu UM

12 Juni 2013

Mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa Doudou Diène ameeleza wasiwasi wake juu ya mparaganyiko wa kisiasa nchini Côte d’Ivoire akitaka kuwepo kwa usawa wa haki ndani ya nchi hiyo ambayo ameielezea sasa ina mgawanyiko baada ya msukosuko. 

Akiwasilisha ripoti yake kwenye kikao cha 23 cha Baraza la haki za binadamu mjini Geneva, Uswisi, Diène amesema harakati za kujikwamua kutoka mzozo wa kisiasa nchini humo zinakabiliwa na changamoto kubwa ya uwepo wa haki.

Amesema licha ya kwamba kuna mwelekeo mzuri wa matumaini lakini bado changamoto ya haki ni kubwa akitolea mfano kuhamishwa kwa watuhumiwa wa vurugu za baada ya uchaguzi kwenda mji wa Abidjani. Bwana Diene amesema hatua hiyo ni dalili nzuri ya kujali lakini watuhumiwa hao pia wapatiwe haki ya kujitetea, kufikishwa mahakamani au kuachiwa huru.

Kuhusu maridhiano, ametaka tume ya kitaifa ya maridhiano na usuluhishi iongezewe muda baada ya ukomo mwezi Septemba mwaka huu ili iweze kuhitimisha majukumu yake kwa mujibu wa hadidu za rejea.