Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mipango ya maendeleo izingatie utamaduni wa watu: UM

Mipango ya maendeleo izingatie utamaduni wa watu: UM

Hapa mjini New York, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekutana kujadili uhusiano kati ya utamaduni na maendeleo. Joshua Mmali amekuwa akiufuatilia mjadala huo.

TAARIFA YA JOSHUA MMALI

Katika hotuba yake ya kufungua kikao cha leo cha Baraza Kuu, rais wa BarazahiloVuk Jeremic, ametoa wito kwa nchi wanachama ziifanye ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 jambo la kipaumbele, akisema anaamini kutekelezwa kwake kikamilifu kutasaidia kuleta pamoja tamaduni tofauti duniani, na kuziwezesha kutangamana vyema zaidi. Amesema muhimu zaidi katika uhusiano wa tamaduni ni kushauriana kwa heshima, na kuufanya daraja ya ushirikiano katika kutimiza ajenda ya maendeleo endelevu. 

“Naamini kuwa kujenga daraja imara na za kudumu baina ya tamaduni za mwanadamu kutasaidia kukabiliana na tofauti nyingi zinazosimama kwenye barabara ya kuendelea mbele kwa pamoja kama jumuiya ya mataifa tofauti yalounganishwa kwa ajili ya kutafuta kufikia maendeleo endelevu kwa wote.”

 Akiongea katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema wakati ajenda ya maendeleo baada ya 2015 ikibuniwa, ni lazima ikumbukwe kuwa hakuna mfumo wa maendeleo unaowafaa watu wote. Amesema ni lazima kila muktadha uzingatiwe, kwani mipango mingi ya maendeleo haijafanikiwa kwa sababu haikuzingatia muktadha wa utamaduni wa watu.

 “Maendeleo hayajaangazia watu ipasavyo. Ili kuwajumuisha watu, tunatakiwa kuelewa na kuheshimu utamaduni wao. Hii inamaanisha kuchagiza mashauriano, kusikiliza sauti za watu binafsi, na kuhakikisha kuwa haki za binadamu ni sehemu muhimu ya maendeleo endelevu”