Ukanda wa Sahel wakabiliwa na njaa, magonjwa na vita -Piper

11 Juni 2013

Mratibu wa misada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika ukanda wa Sahel Robert Piper amesema ukanda huo unakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa chakula, hali mbaya ya usalama na magonjwa na kwamba kiasi cha dola bilioni moja nukta saba kinahitajika kusaidia watu wa eneo hilo.

Akiongea na waandishi wa habari mjini New York Bwana Piper amesema licha ya mvua nyingi kunyesha mwaka huu katika eneo hilo, ikilinganishwa na mwaka jana, maafa ya sasa yanatokana na ukame mkubwa uliokumba eneo hilo, huku akitaja pia idadi kubwa ya watu, mabadiliko ya tabianchi na  hali mbaya ya usalama kuchangia hali hiyo.

Bwana Piper amesema mathalani nchini Mali hali mbaya ya mapigano imesababisha utapiamlo, uwepo wa wakimbizi na pia nchi hiyo inaendelea kuathirika na ukame wa mwaka jana licha ya mwaka huu mvua kubwa kunyesha katika ukanda wa Sahel kwa ujumla.

Nchini Chad amesema nchi hiyo ina mzigo wa  wakimbizi wa ndani nusu milioni, huku pia hali mbaya ya chakula na usalama ikizikumba Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini, Chad na Niger, ambako amesema familia zinashindwa kupeleka watoto shuleni na kutumia theluthi mbili ya kipato kwa ajili ya chakula, na wakati mwingine hulazimika kula mbegu za mazao badala ya kuzihifadhi kwa ajili ya kilimo.