UM wahofia watoto 53 DRC kusajiliwa tena na waasi wa M23

10 Juni 2013

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, MONUSO pamoja na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu watoto katika vita vya silaha, Leila Zerrougui, wameelezea wasiwasi kufuatia ripoti zinazoonyesha kuwa yapata watoto 53 wapo katika hatari ya kusajiliwa tena na kundi la waasi wa M23, kwenye eneo la Nyiragongo, mkoa wa Kivu Kaskazini, DRC.Watoto hao 53 walio hatarini walikuwa miongoni mwa watoto 70 waliosajiliwa na M23 katika maeneo ya Nyiragongo na Rutshuru, na walijinusurisha kutoka kwa waasi hao wakati wa mapigano kati ya makundi ya Bosco Ntaganda na Sultani Makenga mnamo mwezi Februari 2013.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu katika DRC, Roger Meece, amelaani vikali usajili na utumikishaji wa watoto vitani, pamoja na ukiukwaji mwingine wa haki za watoto unaotekelezwa na M23 na makundi mengine yenye silaha, na kuyataka yaache mara moja uhalifu huo.

Naye Bi Leila Zerrougui amewakumbusha viongozi wa makundi hayo kuwa watawajibishwa binafsi kwa ukiukwaji wowote wa haki za watoto.