WHO yataja maadui wa afya ya umma duniani

10 Juni 2013

Mkutano wa Nane wa dunia kuhusu uboreshaji wa afya umeanza Jumatatu huko Finland ukimulika zaidi mwelekeo wa afya ya jamii ambao ni msingi wa jamii kuwa na afya bora. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi. 

(TAARIFA YA ASSUMPTA)

Mkutano huo ulioandaliwa kwa pamoja na WHO na Finland unaangalia kile ambacho serikali zinapaswa kufanya ili kuboresha afya ya umma.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Margaret Chan amesema harakati za kuwezesha binadamu kufuata mfumo wa maisha wenye afya zinakumbana na upinzani usio rafiki, akitaka nguvu za soko.

Amewaeleza wajumbe kuwa jitihada za kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, moyo zinakinzana na maslahi ya kibiashara ya waendeshaji wakubwa na kwa mtazamo wako hiyo ni changamoto kubwa ya uboreshaji wa afya.

(SAUTI YA Dkt. CHAN)

Kama machapisho mapya yanavyobainisha, siyo tu kampuni za tumbaku, bali afya ya jamii inakabiliana pia na vyakula, soda na pombe. Sekta hizi zote zinahofia sheria na zinajilinda kwa kutumia mbinu zinazofanana. Mbinu hizo ni pamoja na zawadi, misaada na michango inayoonekana kuwa na thamani na kufanya sekta hizo zionekane kuwa zinathamini raia katika macho ya wanasiasa na umma.”

Dkt. Chan amesema tatizo kubwa ni ukosefu wa utashi wa kisiasa katika kudhibiti wafanyabiashara wakubwa na hivyo amesema kwa WHO utungaji wa sera za afya unapaswa kulindwa dhidi ya maslahi ya kibiashara au ya watu wachache.