Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN women yamulika ugatuaji madaraka kwa maslahi ya wote

UN women yamulika ugatuaji madaraka kwa maslahi ya wote

Mtandao wa Umoja wa Mataifa unaohusika na ustawi wa wanawake umeanza mkutano wa siku mbili nchini Tanzania kwa ajili ya kutathmini hatua za maendeleo na namna nchi za Afrika zilivyopiga hatua kuteleza mpango wa ugatuaji madaraka.

George Njogopa na taarifa zaidi

Mkutano huo ambao umewaleta pamoja wajumbe kutoka nchi za Msumbiji, Rwanda, Sierra Leone na Senegal na wenyji Tanzania unajumuisha pia wataalamu wa masuala ya jinsia kutoka nchi za Marekani, Canada, Afrika Kusin na Ubelgiji.

Pamoja na mambo mengine, wataalamu hao wanamulika kwa kina utekelezwaji wa mpango ulioasisiwa na Umoja wa Mataifa unaotaka wanawake kupewa nafasi ikiwemo kwenye mabaraza ya maamuzi.

Hii ikiwa pamoja na kuanzisha kampeni zinazohimiza mageuzi katika sera na sheria ambazo hazitoa fursa sawa kwa wanawake kujitokeza kwenye safu za uongozi.

Licha ya kwamba ripoti nyingi za kimaendeleo kuwataja wanawake kuwa nguvu muhimu ya uchangiaji ukuzaji uchumi lakini hata hivyo katika maeneo mengine barani afrika wanawake bado wanachukuliwa kama watu wa daraja la chini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkutano huo, Naibu Waziri anayehusika na tawala za mikoa, Aggrey Mwanri alikariri madhira yanayowakumba wanawake.

(SAUTI YA AGGREY MWANRI)

Huu ni mkutano wa kwanza kufanyika chini ya kivuli cha Umoja wa Mataifa ukiwa na shabaha ya kutoa msukumo kwa tawala za mikoa kuhakikisha mipango yake ya kimaendeleo inazingatia usawa wa kijinsia.

Kumekuwa na mipango mbalimbali ya kimataifa inayohimiza usawa wa kijinsia ikiwemo ule mpango ulioasisiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya maendeleo kusin mwa Afrika SADC ambao unataka kuwepo kwa uwakilishi wa asilimia 50 kwa 50 kwenye bunge.

Akizungumzia harakati za wanawake kushiriki kwenye mabaraza ya maamuzi, Bi Mary Ukomu ambaye ni Mtendaji mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa unaozingatia usawa wa kijinsia na ugatuaji madaraka amesema kuwa.

(SAUTI YA MARY UKOMU)

Mwishoni mwa mkutano wao, wajumbe wanatazamia kupitisha maazimio ya pamoja.