Mkutano kuhusu Syria sasa kufanyika penginepo Julai na si mwezi huu: Brahimi

5 Juni 2013

Mkutano wa kimataifa kuhusu Syria uliokuwa ufanyike mwezi huu huko Geneva, sasa utafanyika penginepo mwezi ujao kwa sababu maandalizi hayajakamilika.

Taarifa hizo zimetolewa na mjumbe maalum wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na nchi za kiarabu, Lakhdar Brahimi alipokutana na waandishi wa habari baada ya mazungumzo ya utatu ya maandalizi baina ya Urusi, Marekani na yeye mwenyewe.

Bwana Brahimi amesema wamelazimika kusogeza mbele kwa kuwa bado kuna mambo mengi ya kufanya ili mkutano huo uweze kufanyika, mathalani makubaliano kuhusu uwakilishi kutoka upande wa upinzani nchini Syria. Hata hivyo wamekubaliana msimamizi mkuu wa mkutano awe Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Amesema kwa pamoja wamekiri kuwa hali nchini Syria ni mbaya na kwamba janga linaloendelea linapaswa kumalizika kwa maslahi ya Syria na wananchi wake na hivyo kwa wiki zijazo wataongeza kasi ya kushughulikia suala hilo ili wakutane tena tarehe 25 mwezi huu mjini Geneva.

Lengo la mkutano wa kimataifa kuhusu Syria ni kuleta maafikiano kati ya serikali ya Syria na upinzani katika kufanikisha suluhisho la kisiasa kwenye mzozo huo kwa kuzingatia taarifa ya pamoja ya tarehe 30 Juni mwaka 2012 hususan kipindi cha mpito.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter