Raia Elfu Nne wa Eritrea hukimbia nchi yao kila mwezi

5 Juni 2013

Hali ya usimamizi wa haki za binadamu nchini Eritrea inazidi kuporomoka kila uchwao na hivyo ndivyo baraza la haki za binadamu limeelezwa huko Geneva, Uswisi na mtaalamu huru wa haki za binadamu na kusababisha maelfu ya raia kukimbia nchi hiyo. Ripoti ya Alice Kariuki inafafanua zaidi.

 (RIPOTI YA ALICE KARIUKI)

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Eritrea Sheila Keetharuth ameliambia baraza la haki za binadamu kuwa hali nchini humo si shwari na kwamba sera ya kujiunga na jeshi kwa mujibu wa sheria haina tofauti na kulazimisha watu kufanya kazi bila ujira.

Amesema raia takribani Elfu Nne wa Eritrea wengi wao wakiwa watoto walio peke yao wanakimbia nchi hiyo kila mwezi kukwepa maonevu na ukosefu wa uhuru.

Sheila amesema licha ya kwamba Eritrea iko kwenye mwelekeo wa kutimiza malengo Sita kati ya Nane ya Milenia, harakati hizo ziende sambamba na heshima kwa haki za binadamu na uhuru wa msingi.

(SAUTI YA SHEILA)

Hata hivyo Eritrea haitambui mamlaka ya mtaalamu huyo huru na imekataa kumwalika nchini humo.