Madhila ya kubakwa ni machungu kama ilivyo risasi: Bangura

4 Juni 2013

Mjini New York hii leo, ubalozi wa Ireland uliandaa mjadala kuhusu nafasi ya wanawake katika ujenzi wa amani hususan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC ambapo washiriki wamezungumza vile ambavyo dunia hivi sasa inatambua nafasi ya wanawake siyo tu kama wahanga wa mizozo ya vita bali pia wanaharakati ambao wanaweza kuleta mabadiliko. Miongoni mwa washiriki alikuwa Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili dhidi ya wanawake katika maeneo ya vita, Zainab Hawa Bangura ambaye amesema licha ya kwamba vitabu vya historia vimekuwa kimya kuhusu madhara ya ubakaji kwenye vita, wanawake na watoto wa kike wamekuwa wakifahamu fika mapigano yanayokumba siyo tu jamii zao bali pia miili yao. Bi Bangura amesema ukatili wa kingono una madhara makubwa kama ilivyo risasi. Hata hivyo amesema wakati wa sasa kuna mabadiliko makubwa..

 (SAUTI YA BANGURA)

 

Bi. Bangura amesisitiza suala la uchunguzi wa kina kwa watu wanaoajiriwa jeshini ili kuepusha wahusika wa ukatili wa kingono vitani kujumuisha kwenye majeshi ya kitaifa huku akisifu serikali ya DRC kwa kuweka mpango wa kuchunguza watendaji wapya.

Mary Robinson ambaye ni mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Maziwa Makuu amesema ushauri wa kina na wa dhati kuhusu nafasi ya wanawake kwenye ujenzi wa amani kutawezesha kuwepo kwa amani ya kudumu kwenye ukanda huo.