Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusaini mkataba wa biashara ya silaha kwa maslahi ya wote: Ban

Tusaini mkataba wa biashara ya silaha kwa maslahi ya wote: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezitaka nchi wanachama wa umoja huo kujitokeza kwa wingi kutia saini mkataba wa kimataifa kuhusu biashara ya silaha, ATT, ulioanza kutiwa saini leo baada ya kupitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Aprili mwaka huu.

Akizungumza mjini New York, Marekani siku ya Jumatatu baada ya kuanza kutekelezwa kwa mkataba huo, Bwana Ban amesema hatua hiyo ni muhimu kwa amani, usalama na maendeleo duniani, akisema ni vyema nchi zinazoongoza kwa biashara ya silaha duniani zikaonyesha mfano kwa kusaini mkataba huo.

 

(SAUTI BAN)

“Nazisihi nchi zote zifanye vivyo hivyo, hususan zile zinazoongoza kwa biashara ya silaha. Dunia nzima inatizama wafanyabiashara wa silaha, watengenezaji na serikali kuliko wakati wowote ule. Nazisihi serikali kupitisha sheria na kanuni kwa mujibu wa mkataba huo ili uweze kuwa na nguvu kwa usalama na maendeleo ya wote.”

Bwana Ban huku akipongeza nchi ambazo tayari zimesaini mkataba huo, amesema kwa upande wake Umoja wa Mataifa uko tayari kutoa usaidizi wowote ule kufanikisha utekelezaji wa mkataba huo wa biashara ya silaha.